Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Waziri Aweso azindua mradi wa Maji Busenda

Waziri Aweso azindua mradi wa Maji Busenda

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amezindua mradi wa maji Busenda wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga ambao umegharimu kiasi cha Shilingi 344,480,060 za Kitanzania ikiwa ni fedha zinazotokana na Mpango wa Malipo kwa Matokeo (PforR) huku akimpongeza Mhandisi wa RUWASA mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela, kwa kusimamia mradi huo kwa weledi.

Waziri Aweso alisema ujenzi wa mradi huo ni kutokana na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya Majisafi na Salama na ya uhakika katika kijiji cha Busenda. Wananchi wapatao 3,551 watanufaika na huduma ya majisafi na salama kutoka katika mradi huo.

Aidha, mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani ameishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao utasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji. Kukamilika kwa mradi huo, kutasaidia wananchi kupata wa muda wa kushiriki shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii, na kupunguza maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Utekelezaji wa mradi huo umefanywa na wataalamu wa ndani wa RUWASA kwa mfumo wa ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 10 Machi, 2023 na kukamilika tarehe 5 Septemba, 2023.