Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Kuhusu RUWASA

Kuanzishwa

Sheria Na.5 ya mwaka 2019 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, pamoja na mambo mengine, ilianzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambayo ilichukua majukumu yaliyokuwa hapo awali yamekabidhiwa kwa OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Majukumu yaliyohamishwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwenye jamii za watu waishio maeneo ya vijijini, miji midogo na Makao Makuu ya Wilaya.

Sheria Na.5 ya mwaka 2019 imehamisha uwajibikaji wa maafisa wanaohusika na utoaji wa huduma ya maji kutoka OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda Wizara ya Maji. Wakala mpya iliyoanzishwa (RUWASA) ina  ofisi ngazi za Makao Makuu Dodoma, Mikoa na Wilaya. Hii ni tofauti na muundo wa hapo awali ambao ulikuwa unajumuisha ofisi katika ngazi ya Serikali za Mitaa (LGAs) na Sekretarieti za mikoa (RSs).

RUWASA ilianza kazi tarehe 1 Julai 2019, na mpaka sasa wakala hii inahudumia mikoa 25 ya Tanzania Bara isipokuwa Dar Es Salaam.

Muundo wa RUWASA:

Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019, mfumo wa RUWASA wa utoaji wa huduma za maji vijijini na usafi wa mazingira una muundo ufuatao:

Waziri Mwenye Dhamana ya Maji: Pamoja na mambo mengine, Waziri wa Maji atakuwa na jukumu la kutekeleza sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali katika kufanikisha miradi na huduma ya maji na usafi wa mazingira katika maeneo ya vijijini.

Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA: Bodi itakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa majukumu na utendaji wote wa RUWASA juu ya masuala ya huduma ya maji vijijini pamoja na kumshauri Waziri mwenye dhamana.

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASAMkurugenzi mkuu pamoja na timu yake watakuwa na jukumu la kufanya shughuli za kila siku za RUWASA wakiwa na lengo la kufikisha maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira kwenye maeneo ya vijijini. Ili kuongeza ufanisi wa ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, patakuwa na ofisi za RUWASA katika ngazi ya Mkoa na Wilaya.

Ofisi za RUWASA ngazi ya Mkoa: Meneja wa RUWASA mkoa, atakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na  huduma za maji na usafi wa mazingira. Aidha, atakuwa na jukumu la kutoa msaada wa kiufundi kwa wilaya husika; 

Ofisi za RUWASA ngazi ya WilayaMeneja wa Wilaya atakuwa mtekelezaji mkuu wa miradi ya usambazaji maji na usafi wa mazingira katika wilaya yake. Aidha, ofisi hizi zitakuwa na jukumu la msingi la kuwezesha Jumuiya za Usimamizi wa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kuendeleza utoaji wa huduma.

Vyombo vya Utoaji wa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs): Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) zitaanzishwa kwa ridhaa ya jamii ya wananchi walio wengi kama chombo huru chenye kujitegemea. CBWSO inaweza kuwa ni;

 i) Chama cha Watumia maji;

ii) Bodi ya Wadhamini (wa Maji);

iii) Chama cha Ushirika;

iv) Asasi zisizokuwa za Serikali;

v) Kampuni; au

vi) Chombo kingine chochote kitakachopitishwa na Waziri mwenye dhamana.
 Vyombo vya Utoaji wa  Huduma ya Maji 
Ngazi ya Jamii (CBWSOs) vitakuwa na wajibu wa kusimamia, kuendesha na kukarabati miradi ya maji. Kimsingi vyombo hivi vitakuwa na jukumu la kuhakikisha huduma za maji vijijini zinakuwa endelevu.