Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Huduma

HUDUMA ZA USAMBAZAJI MAJI

Kutokana na Sheria ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Namba 5 ya 2019, RUWASA imepewa jukumu la kuhakikisha jamii za wananchi waishio maeneo ya vijijini ndani ya Tanzania Bara zinapata huduma ya maji safi na salama. Hata hivyo, RUWASA inawajibika kutoa huduma za maji katika maeneo yote ambayo RUWASA itakabidhiwa na Waziri mwenye dhamana ya sekta ya maji.

Huduma za maji katika maeneo ya vijijini husimamiwa na kuendeshwa na Jumuiya za Usimamizi wa Huduma za Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) chini ya usimamizi wa RUWASA katika ngazi ya Wilaya. Ili kuhakikisha uendelevu wa huduma za usambazaji maji, CBWSO hukusanya tozo za maji kutoka kwa jamii kama ilivyojadiliwa na kukubaliwa katika vyombo husika.

Aidha, CBWSO inawajibika katika kufanya matengenezo ya mradi ili kuhakikisha jamii inapata huduma ya maji safi na salama kila siku.

HUDUMA ZA USAFI WA MAZINGIRA

RUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na OR-TAMISEMI kwa pamoja zina jukumu la kuhakikisha huduma za usafi wa mazingira zinazingatiwa na kutekelezwa katika maeneo ya vijijini. Hata hivyo, RUWASA inapaswa kuchochea na kuhamasisha jamii za vijijini kuzingatia usafi wa mazingira pamoja na kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Wizara ya Maji na RUWASA zinawajibika kutoa miongozo na kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya huduma za usafi wa mazingira maeneo ya vijijini.