Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Serikali Kuanza utekelezaji mradi wa maji vijiji 57 Wilaya ya  kyerwa

Serikali Kuanza utekelezaji mradi wa maji vijiji 57 Wilaya ya kyerwa

SERIKALI KUANZA  UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI VIJIJI 57 KYERWA

WANANCHI  WAPATAO ELFU  83,000 KUNUFAIKA 

Naibu  Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb)  amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji katika vijiji 57 Wilayani Kyerwa. Amesema  hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo unaendelea katika vijiji 27 ambavyo ni Nkwenda, Rwabwere, Karongo, Nyamiaga, Nyakatera, Kagu, Masheshe, Nyamweza, Kaikoti, Iteera, Muleba, Chanya, Kimuli, Rwanyango, Chakalisa, Kikukuru, Omukitembe, Karambi, Rwele, Rubilizi, Mukunyu, Kitwechenkura, Rukuraijo, Makazi, Kibimba, Nyakatete na Mabira. 

Mhandisi Mahundi ameyasema hayo leo Januari 30, 2024  bungeni jijini  Dodoma  wakati akijibu swali la mbunge wa  jimbo la Kyerwa Innocent  Bilakwate  aliyetaka kufahamu lini Mradi wa maji wa Vijiji 57 ambao utaanzia Kyerwa, Nyakatuntu mpaka Kamuli Wilayani Kyerwa utaanza ili Wananchi wapate maji. 

Mhandisi Mahundi amesema kazi zinazotekelezwa katika miradi hiyo ni pamoja na ujenzi Matenki Matano (5) yenye jumla ya ujazo wa lita 1,450,000, ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 110, ujenzi wa Vituo 102 na Vioski 18. Utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 80 na inatarajiwa kukamilika Mwezi Mei, 2024 na kuwanufaisha wananchi wapatao 83,000. Miradi katika Vijiji 30 vilivyobaki itatekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/25