Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Huduma ya Majisafi Vijijini sasa asilimia 77

Huduma ya Majisafi Vijijini sasa asilimia 77

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi ya bomba vijijini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 74.5 mwezi Desemba, 2021 hadi kufikia wastani wa asilimia 77 mwezi Desemba, 2022. Kiwango kilichoongezeka kimetokana na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi 586 yenye vituo 5,748 vya kuchotea maji vinavyonufaisha wananchi wapatao 4,086,442 kwenye vijiji 1,293.

Waziri Aweso ameyasema hayo Mei 10, 2023 wakati ikiwasilisha Makadirio ya Mpango wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Bungeni jijini Dodoma. “Hali hiyo inafanya jumla ya wananchi wa vijijini wanaopata huduma ya maji kuwa 30,209,409” alisema Waziri Aweso.

Alisema lengo la Serikali ni kuwapatia wananchi waishio vijijini huduma ya majisafi na salama kufikia zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025 na kwamba katika kutimiza lengo hilo, Serikali imeendelea kujenga, kukarabati, na kupanua mitandao ya kusambaza maji pamoja na kuimarisha usimamizi wa huduma ya maji.

Katika wasilisho lake, Waziri Aweso ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 756.2 kwa ajili ya matumizi ya Wizara hiyo kwa ujao wa fedha ambapo Wabunge wataendelea na majadiliano hadi Mei 11, 2023 kabla ya mtoa hoja ambaye ni Mhe. Aweso kuhitimisha kwa kujibu hoja zilizotolewa na Wabunge hao.