Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

RUWASA yawafunda watumishi wapya

RUWASA yawafunda watumishi wapya

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement KIVEGALO amewataka watumishi wapya walioajiriwa kutumikia taasisi hiyo kuchapa kazi kwa bidii, uadilifu, na weledi ili kufikia lengo kuu la kuanzishwa kwa Wakala huyo ambalo ni kuhakikisha wakazi wa Vijijini wanapata huduma ya Majisafi, salama, na yenye kutosheleza.

Mhandisi KIVEGALO ametoa wito huo Oktoba 31, 2022 wakati wa semina ya mafunzo kwa watumishi hao wapya inayofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu  aliwataka watumishi hao kuwa waaminifu na wabunifu kwa manufaa ya taasisi hiyo aliyoitaja kuwa bado changa na inahitaji mchango wa kila mtumishi katika kuijenga. 

“Tunataka RUWASA iwe namba moja katika kila nyanja ikiwemo ubora wa huduma zetu, nidhamu, weledi, na uadilifu” alisema KIVEGALO.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mhandisi KIVEGALO ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi, aliipongeza idara ya Utawala na Rasilimaliwatu kwa kuandaa mafunzo ya awali kwa watumishi wapya na kwamba yatawajengea msingi imara wa kazi na kuifahamu taasisi na utamaduni wake pamoja na Sera, Sheria, na Miongozo inayoisimamia taasisi ya RUWASA.

Awali akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo, Bwai Biseko ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa RUWASA, alisema mafunzo hayo yanajumuisha watumishi wapya 215 walioajiriwa hivi karibuni na kwamba katika awamu ya kwanza yamejumuisha watumishi 71.