Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Miradi ya RUWASA yaendelea kung'ara Mbio za Mwenge - 2023

Miradi ya RUWASA yaendelea kung'ara Mbio za Mwenge - 2023

WANANCHI 5,621 wa vijiji vya Kizanda na Mayo, Kata ya Mayo, Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wanatarajia kunufaika na mradi wa maji wa Mayo. Hayo yamesemwa Juni 13, 2023 na Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim wakati wa mbio za Mwenge zilipofika katika mradi huo kwa ajili ya kukagua na kuufungua.

Mhandisi Sizinga amesema ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi huo ni miongoni mwa kazi zilizokamilika na kwamba zimesimamiwa na Ofisi ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19. Amesema mradi huo uliwekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022, na ulitekelezwa na Mkandarasi Mbesso Construction Co. Ltd wa Dar es Salaam kwa mkataba ulioanza utekelezaji wake Februari Mosi, 2022 na kukamilika Septemba 30, 2022.

“Utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 kulingana na mkataba, na unategemea kunufaisha wakazi 5,621 wanaoishi kwenye vijiji vya Kizanda na Mayo na umegharimu zaidi ya shilingi milioni 430 (430,909,580) ambazo ni gharama za mkandarasi katika ujenzi wa miundombinu, na amelipwa fedha zote,” alisema Sizinga. Sizinga alisema kazi zilizofanyika kwenye mradi huo ni chanzo kipya cha maji, ufyekaji wa njia za bomba kuu, tenki la maji lenye ujazo wa lita 90,000, vituo vya kuchotea maji (vilula) vinane, vituo saba vya nyongeza, uchimbaji wa mitaro ya bomba yenye urefu wa mita 15,000, ulazaji na uungaji mabomba mita 15,500, ujenzi wa chemba pamoja na vifaa vyake.

“RUWASA tunatoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha za miradi ya maendeleo, tutazisimamia vizuri ili ziweze kuleta tija kwa wananchi na kufikia malengo yaliyokusudiwa,”alisema.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim ameupongeza mradi huo ambapo amesema umejengwa kwa viwango, na utanufaisha wananchi wengi.

Kwa msaada wa Times Majira