Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

RUWASA yaeleza mafanikio tangu kuanzishwa

RUWASA yaeleza mafanikio tangu kuanzishwa

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Bwai Biseko ameelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa RUWASA ambapo amesema hadi kufikia Desemba 2022, jumla ya miradi 2,273 ya miundombinu ilikuwa imejengwa na kukamilika kupitia fedha za ndani na wadau wa Maendeleo.

Biseko aliyasema hayo wakati ukitoa taarifa ya utendaji kazi ya RUWASA kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya RUWASA iliyofanyika Juni 27, 2023 katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma na kuongozwa na Mhe. Jumaa Aweso,  Waziri wa Maji.

Mkurugenzi huyo alisema miradi hiyo inanufaisha wanachi 11,641,230 katika vijiji 4,809 ambapo katika kipindi hicho, ujenzi wa mabwawa saba ulikamilika na jumla ya visima 947 vilichimbwa.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi September 2022, RUWASA ilifanikiwa kuunda na kusajili Vyombo vya Watumia Maji ngazi ya jamii (CBWSOs) 2,524 na zimeweza kuajiri watalaam 5,586 wa fani za ufundi, uhasibu na kada saidizi ili kuwa na uendelevu wa huduma ya maji vijijini.

“Mheshimiwa Mgeni Rasmi, vilevile, nikushukuru wewe pamoja na uongozi wa Wizara ya Maji kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa majukumu ya RUWASA, kiasi cha Sh.995,638,503,970 kati ya Sh. 1,044,588,249,042 zilizotengwa ambayo ni sawa na asilimia 95 ya bajeti ya RUWASA kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2021/2022, fedha ambazo zimewezesha kupatikana kwa mafanikio yaliyotajwa hapo juu” alisema katika taarifa yake.

Alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024, RUWASA imepanga kutekeleza jumla ya miradi ya maji vijijini 1,546 ikihusisha miradi ya ujenzi wa mabwawa ya kuhifadhi maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Tangu kuanzishwa kwa RUWASA, huduma ya majisafi vijijini imeongezeka kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 77 kwa sasa, ambapo lengo ni kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama Tawala.