Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Rais Samia aipa kongole Sekta ya Maji

Rais Samia aipa kongole Sekta ya Maji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua Skimu ya Maji ya Kakonko - Kiziguzigu inayotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini [RUWASA] kwa kushirikiana na Taasisi ya Enabel kutoka nchini Ubelgiji. Skimu hiyo inatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 4 na inatarajiwa kunufaisha kata Nne za Kakonko Mjini, Kiziguzigu, Kasuga na Kanyonza zenye jumla ya vijiji kumi na vinne (14).

Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maji katika eneo la mradi mara baada ya uzinduzi huo Mhe. Samia amewapongeza watumishi hao kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji. Amesema mabadiliko chanya yanayoonekana kupitia Wizara ya Maji yanatoa matumaini kuwa serikali itafikia malengo yaliyokusudiwa katika sekta ya maji.

Zamani huko nilikuwa na ugomvi na watu wa maji''. Kwa sasa,  watu wa maji ni marafiki zangu kweli kweli. Wizara imebadilika. Taasisi zilizoko chini ya wizara zimebadilika. Kazi inafanywa kwelikweli Naomba muendelee hivyo hivyo. Amesema Rais Samia. 

Awali akimkaribisha Mhe. Rais Kuzindua mradi huo, Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema Mradi wa Kakonko - Kiziguzigu utakapokamilika katika vijiji vyote 14 utahudumia wakazi wapatao 65,010. Nia ni kufikia wakazi wapatao 132,425 ifikapo mwaka 2042 ambao ndio kipindi cha usanifu wa mradi.

Awamu ya kwanza ya mradi imekamilika katika vijiji vya Kakonko, Itumbiko, Mbizi, Kiziguzigu, Kiyobera, Ruyenzi, Kabingo na Kasuga ambapo kwa sasa wananchi wanapata huduma ya maji.

Aidha,  mradi huo umeongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 51 hadi zaidi ya asilimia 70 huku mgao wa maji ukipungua kutoka saa 12 hadi saa 5 kwa siku. Amesema mipango inaendelea ikiwemo kupanua mradi huo ilii huduma ya maji katika wilaya hiyo ifikie asilimia mia moja.