Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI

"Maji Bombani"

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso Aimwagia sifa RUWASA

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso Aimwagia sifa RUWASA

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amefungua rasmi mafunzo ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Uongozi, na Taaluma, pamoja na Elimu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Menejimenti ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yanayoendelea katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 27, 2022 ambapo ameimwagia sifa Wakala huyo kwa kasi na ubora wa kutekeleza miradi ya Maji Vijijini na kupelekea sekta ya Maji kuwa namba moja kwa utekelezaji na ubora wa miradi katika ukaguzi uliofanywa wakati wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka huu.

Waziri Aweso ametoa sifa na pongezi hizo wakati wa hatuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo, ambapo amesema silaha na siri ya mafanikio hayo katika sekta anayoiongoza ni kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, uadilifu, na kwa kuzingatia weledi.

Awali akitoa taarifa ya mafunzo hayo kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement KIVEGALO alisema yamelenga kuongeza weledi, uaminifu na uadilifu zaidi kwa watumishi hao ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi. Sekta ya Maji hususan eneo la Maji Vijijini limepiga hatua nzuri kiasi cha kutangazwa na timu ya wakimbiza Mwenge Kitaifa kuwa namba moja nchini, hivyo hiyo ni changamoto mpya kwake kama mtendaji Mkuu na kwa watumishi wote wa RUWASA kuzidisha bidii ya kazi kwa weledi mkubwa.

Naye Mhe. Kheri James, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo aliisifia RUWASA na sekta ya Maji kwa ujumla kwa mafanikio iliyoyapata katika kipindi kifupi cha uongozi wa Waziri Aweso huku akitoa wito wa kuendeleza umoja, upendo, na ushirikiano kwa watumishi katika kazi ili kuipaisha zaidi sekta hiyo muhimu katika maisha ya Watanzania.