RUWASA ni kifupi cha neno Rural Water Supply and Sanitation Agency (Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini) umeanzishwa chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019. RUWASA ilianza rasmi shughuli zake tarehe 1 Julai, 2019.Makao Makuu ya RUWASA yapo Jijini Dodoma.
Majukumu ya RUWASA yametajwa na kufafanuliwa katika kifungu cha 43 cha Sheria Na. 5 ya mwaka 2019 ya Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira. Kwa ujumla, RUWASA ina wajibu wa kuendeleza miundombinu kwa kufanya ujenzi na usimamizi wa ujenzi wa miradi ya maji na pia kusimamia utoaji wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira vijijini. Katika kutekeleza jukumu hilo, RUWASA inafanya shughuli zifuatazo:-
· Kuandaa mipango, kusanifu miradi ya maji, kujenga na kusimamia uendeshaji wake.
· Kuendeleza vyanzo vya maji kwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi na kuchimba visima pamoja na kujenga mabwawa.
· Kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji vijijini.
· Kusajili, kuratibu, kudhibiti, kufuatilia na kutathmini vyombo vya kijamii vinavyohusika na uendeshaji wa huduma ya maji vijijini
(Community Based Water Supply and Sanitation Organization - CBWSOs) ili kuhakikisha kuwa huduma inakuwa endelevu.
· Kuzijengea uwezo CBWSOs kwa kutoa mafunzo na utaalamu wa uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji vijijini.
· Kuhamasisha jamii na kutoa elimu ya usafi wa mazingira katika ngazi ya kaya na mtu binafsi (sanitation and hygiene) na masuala ya
uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji.
· Kutafuta fedha kwa ajili ya uendeshaji ili kuwezesha RUWASA kutekeleza majukumu yake na kushirikiana na wadau mbalimbali
katika masuala yanayohusu utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira vijijini.
Kuanzishwa
kwa RUWASA ni matokeo ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali ya
Awamu ya Tano kwenye Sekta ya Maji katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa
huduma ya maji vijijini inaongezeka, inaboreka na inakuwa endelevu. Mabadiliko
hayo, yalifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli tarehe 10 Mei, 2018, ambapo majukumu na uwajibikaji wa watumishi
katika Sekta ya Maji yalihamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) kwenda Wizara ya Maji.
Katika ngazi ya Makao Makuu, RUWASA ina ofisi katika ngazi za Mikoa na Wilaya ambazo zinaongozwa na Mameneja wa Mikoa, na Mameneja wa Wilaya,na chini yao, kuna watumishi wa fani mbalimbali. Kwa sasa, RUWASA inafanyakazi katika Mikoa 25 kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Mkoa wa Dar es Salaam unahudumiwa na DAWASA katika maeneo yote na hivyo, haupo chini ya RUWASA.
●RUWASA inawajibika kutoa huduma katika maeneo ya vijinini na mijini ambayo hayahudumiwi na Mamlaka za Maji.
●Mamlaka za Maji zinawajibika kutoa huduma katika maeneo ya mijini au / na vijijini yaliyotangazwa na waziri mwenye dhamana na Sekta ya Maji.
●Katika maeneo ambayo hayajaundiwa Mamlaka za Maji huduma inatolewa kupitia Vyombo vya kijamii (CBWSOs)